Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ripoti ya Washington Post imesema Kanali Assimi Goita aliyejitokeza Alkhamisi iliyopita kama kinara wa Baraza la la Kijeshi linalotawala Mali baaba ya mapinduzi ya kijeshi, alifanya kazi kwa miaka mingi na kikosi maalumu cha Marekani huko magharibi mwa Afrika.
Vilevile maafisa wa jeshi la Mali ambao hawakutaka majina yao yatajwe wamesema kuwa, Kanali Assimi Goita alikuwa akifanya mazungumzo mara kwa mara na maafisa wa jeshi la Marekani na kuhudhuria mazoezi yao ya kijeshi.
Kanali Assimi Goita ambaye pia alipata mafunzo ya kijeshi katika nchi za Ujerumani na Ufaransa, alikuwa akiongoza kikosi maalumu cha jeshi la Mali katika eneo la katikati mwa nchi hiyo linalosumbuliwa na machafuko.
Takwimu za Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) pia zinaonesha kuwa, Kanali Assimi Goita alishiriki katika mafunzo ya kijeshi yaliyosimamiwa na Marekani huko magharibi mwa Afrika maarufu kwa jina la Flintock na alihudhuria kongamano la operesheni makhsusi lililofanyika katika kambi ya Jeshi la Anga ya MacDill katika jimbo la Florida.
Gazeti la Washington Post pia limeripoti kuwa kiongozi wa mapinduzi ya mwaka 2012 nchini Mali, Kapteni Amadou Sanogo, pia alipewa mafunzo ya kijeshi na Marekani.
Ripoti ya Washington Post imesisitiza kuwa, wanajeshi wengi walioshiriki katika mapinduzi ya juzi nchini Mali wamepewa mafunzo ya kijeshi nchini Marekani.
Nchi za Afrika zimepinga mapinduzi ya serikali halali ya Mali na zimesimamisha uanachama wa nchi hiyo katika Umoja wa Afrika.
342/